Vikwazo vya kibiashara kuondolewa: wadau sekta ya uchumi kenya na tanzania watumie vyema fursa hii
Tanzania na Kenya zimefanikiwa kuondoa vikwazo 12 vya biashara visivyo vya kikodi vilivyokuwa vinatumika kwa miongo kadhaa baina ya nchi hizo mbili.
Hadi sasa jumla ya vikwazo vilivyoondolewa ni 42 kati ya 64, huku vikwazo 30 vikiwa vimeondolewa kwenye mkutano uliofanyika mwezi Mei 2021 mjini Arusha, Tanzania.
Hii inabakiza vikwazo 18 , huku taratibu za kuondoa vikwazo hivyo baina ya nchi hizi mbili zikiwa zinaendelea na inatarajiwa hadi kufikia mwezi Januari 2022 vikwazo vyote vitakuwa vimepatiwa ufumbuzi.
Miongoni mwa vikwazo vilivyokuwa vikisumbua ukuaji na ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili ni; Urasimu katika upitishaji wa bidhaa za mpakani, tozo za ukaguzi, muda wa kibali kwa bidhaa zinazoharibika kama maziwa, taratibu ya sheria za forodha, muda wa kibali cha kuagiza mifugo na vikwazo vingine.
Kwa jicho la pekee, hii ni fursa adhimu na muhimu mno kwa wadau wa sekta ya uchumi katika mataifa yote mawili, yaani Kenya na Tanzania. Wafanyabiashara, wakulima, wasafirishaji pamoja na wawekezaji katika mataifa haya mawili, wanatakiwa kuchangamkia fursa zitokanazo na nchi hizi kwani vikwazo vilivyokuwa vikiathiri uendeshaji wa biashra vimeondolewa kwa kiasi kikubwa:
Wakulima na wafanyabiashra wa zao la mahindi wajikite kuongeza thamani bidhaa zitokanazo na zao hilo; Kwani fursa ya soko limeongezeka kutokana na kikwazo cha mahindi kutoka Tanzania kwenda Kenya kuondolewa. Kama wakulima kutoka Tanzania watahakikisha upatikanaji wa zao hilo kwa kiwango cha kuridhisha na kilichothibitishwa na mamlaka husika, Basi kuna fursa kubwa ya kupata faida katika zao hilo ambalo limeonekana kusuasua kwa bei hapa nchini.
Kwa Tanzani kumeshuhudiwa uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi katika mikoa mbalimabli inayozalisha zao hilo, hadi Serikali kuchukua uamuzi wa kununua mahindi kwa wananchi. Hivyo basi, kutokana na kutolewa kwa vikwazo vya kusafirisha mahindi kwenda nchini Kenya, basi wakulima wajitahidi kulitolea macho soko la nje la nchini Kenya.
Ongezeko la muda wa kibali cha kusafirisha mifugo ukawe chachu katika nchi hizi mbili; Mwanzo kibali cha kusafirisha mifugo katika nchi hizi mbili kilidumu kwa siku kumi na tano pekee (15) huku wafanyabiashara wakilazimika kuingia gharama na mlolongo tena wa kutafuta kibali hicho tena. Lakini kwa sasa kibali hicho kinachotolewa kwa usafirishaji wa mifugo kinadumu kwa siku therathini (30) ,mwezi mmoja. Hii ni fursa katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za mifugo na kupunguwa kwa grarama na taratibu za kufuatilia kibali hicho mara mbili kwa mwezi,ni maoni yangu vibali hivyo kuongezwa muda zaid hata miezi mitatu mitatu, na upatikanaji wake uwe kwa njia rahisi na wezeshi ikiwa tutatumia mifumo rafiki ya tehama.
Kuruhusiwa kwa bidhaa za ngano kwenda nchini Kenya kutoka Tanzania, ni fursa kwa wakulima kuongeza tija katika zao hilo na kuongeza ubora zaidi. Wakati huohuo,hakuna budi kwa wafanyabiashra za usafirishaji kuanza kujinoa na kukidhi matakwa ya kimataifa ili wachangamkie fursa za usafirishaji bidhaa kutoka nchi zote mbili.
Wakati mwingine kuondolewa kwa vikwazo hivi, vinaweza kuonekana kwa watu wengi ni njia ya kuua viwanda vya ndani na kuhatarisha pato kwa wafanyabiashara wa ndani bila kuzingatia chachu itakayoletwa ya kuongeza ufanisi kwenye viwanda vya ndani ili kupeleka bidhaa bora sokoni. Hivyo basi, kuna ulazima wa wadau wa sekta ya uchumi wakiwemo wamiliki wa viwanda na wafanyabiashra kutumia teknolojia za kisasa katika uzalishaji na usindikaji ili kumudu ushindani wa bidhaa . Ni kweli kwamba bidhaa imara yenye ubora itakuwa na wateja sehemu yoyote ile, hivyo ni muhimu kuwa na bidhaa bora na zenye viwango wa kimataifa.
Sambamba na hayo, lazima kuwepo na sheria na utaratibu mkali wa kudhibiti ushindani wa kibiashara usio rafiki; Mfano, baadhi ya makapuni na viwanda kuharibu jina na nyazifa dhidi ya biashara zingine , kufanya mbinu zisizo za kisheria zinazoharibu wateja wa bidhaa Fulani.
Kama ushindani utakuwa ni rafiki na wakuleta chachu katika sekta ya uchumi, basi kutakuwa na tija na maslahi mapana ya kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya nchi hizi mbili.