
Kuelekea Uchumi wa Buluu: SHERIA NA KANUNI ZA UVUVI LAZIMA ZIANGALIWE UPYA
Uchumi wa Buluu unajumuisha shughuli zote za uendelezaji na ukuzaji wa uchumi kwa kupitia matumizi bora ya Rasilimali zote muhimu za Bahari. Mfano; Uvuvi wa aina mbalimbali ukiwemo wa kibiashara na usio wa kibiashra katika kina kirefu na kifupi,Shuguli za usafirishaji majini pamoja na shughuli za uchimbaji wa madini na mafuta baharini.
Ilani ya uchaguzi mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaa mwaka 2020, ilieleza juu ya namna Serikali itakavyoipa kipaumbele sekta ya Uchumi wa Buluu (Blue Economy) kwa mwaka 2020 hadi 2025.
Kupitia sura ya pili; Mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu, Kifungu namba 18 (a) kimebainisha dhamira ya Serikali ya; Kuongeza mchango wa uchumi wa rasilimali za maji (blue economy) katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi, kutengeneza fursa za ajira na kupunguza umasikini wa kipato.
Dhamira hii ni njema na yakutilia mkazo madhubuti. Ili kufikia malengo hayo kwa wakati, basi Serikali haina budi kuzitazama upya sheria, kanuni na vifungu vinavyoibana sekta ya Uvuvi ili kuongeza tija katika taifa kupitia Uchumi wa Buluu.
Sheria za uvuvi za mwaka 2010, ambazo zilifanyiwa marekebisho madogo mwaka 2020 bado zinahitaji marekebisho zaidi ya kimkakati ili kupaisha pato la taifa kupitia sekta hii muhimu. Kulingana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mahimba Ndaki alipozungumza Dodomo Septemba 26, alibainisha sheria ya uvuvi kumezwa na uvuvi wa majini tu na kusahau uvuvi wa kisasa unaotumia vizimba au mabwawa.( Gazeti la NIPASHE 28/9/21 )
Hivyo kuna sababu muhimu ya kupitia upya sheria hizo na kuzifanya ziwe za kurahisiha na kukuza ukuaji na uwekezaji katika sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi , haina budi kupitia sheria na kuweka mikakati ya kutumia mabwawa au vizimba vya kuzalishia na kukuzia viumbe maji:Dunia inaenda kasi kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia. Kuna fursa nyingi kupitia uzalishaji na ukuzaji wa viumbe maji kupitia mabwawa au vizimba. Hii inasaidia sana katika kuongeza tija ya upatikanaji wa viumbe hivyo kama vile; samaki, pweza na kaa. Hivyo kuchangia upatikanaji wa malighafi za kutosha zinazoweza kutumika katika viwanda vya ndani na ziada kuuzwa nje ya nchi na kujipatia kipato kikubwa zaidi kwa taifa na mfanyabiashara mmoja moja.
Taasisi za elimu za juu kwa kushirikiana na Sekta binafsi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi iweke ushirikiano utakaohakikisha upatikanaji wa wataalamu wa kutosha na wenye ufanisi mkubwa; Vyuo vikuu kama UDSM na SUA na vyuo vya kati kama VETA, kunaulazima wa kuweka ushirikiano wa kimkakati wa kufanya kazi kwa pamoja na kwa malengo thabiti na Wizara ya Kilimo na Uvuvi nchini. Hii itasaidia upatikanaji wa wataalamu katika maeneo muhimu ambayo yana uhaba au upungufu wa wataalamu hao.
Wakati huohuo, ushirikiano huo uwe wa kutatua changamoto za wadau wa sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla; kwa kutuma wataalamu waliopo vyuoni au mafunzoni kutembelea maeneo mbalimbali nchini kuelimisha juu ya umuhimu wa kutumia mbinu bora katika uchumi wa buluu. Ikiwemo ya kuanzisha vizimba au mabwawa ya kuzalisha na kukuza viumbe maji na kutumia mbegu bora katika uzalishaji.
Pia Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) iweke ushirikiano wa majukumu ya kikazi utakaorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wa sekta ya uvuvi na uchumi wa buluu kupitia wizara ya kilimo na uvuvi; Kwa kuwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na Wizara ya Kilimo na Uvuvi , kufanya majukumu yao kwa utofauti. Hivyo inawalazimu wadau wa sekta ya uchumi wa buluu na Uvuvi kupata shida ya ufuatiliaji katika sehemu zote mbili. Kama mamlaka hizi mbili muhimu katika sekta hii ya uchumi wa buluu, zitashirikiana kwa pamoja ili kuwezesha wadau na wafanyabiashara kupitia uvuvi na sekta ya uchumi wa buluu kwa ujumla kupata urahisi wa kukamilisha taratibu za kisheria zinazohitajika . Kama vile, leseni za uvuvi na kusajili jina la biashara na kampuni, kama huduma hizi zitapatikana kwa urahisi basi itakuwa chachu ya ukuzaji wa sekta hii muhimu.
Kuweka mazingira rafiki ya usafirishaji na usindikaji wa bidhaa zitokanazo na Uchumi wa buluu; Lazima mazingira wezeshi yanayosaidia wavuvi na wadau katika uchumi wa buluu yawekwe, ili kuwezesha uchakataji na usafirishaji wa viumbe maji watokanao na uchumi wa buluu. Mfano, kuna hitaji kubwa la majongoo wa baharini katika nchi ya China ambapo kuna soko la uhakika na lenye faida kubwa. Hivyo, Serikali kupitia mamlaka husika ziweke mazingira wezeshi, ikiwemo kupunguza ushuru na kodi katika bidhaa zitokanazo na viumbe maji kama; samaki, jongoo na pweza.
Taasisi za fedha nchini ziweke mkakati wa pamoja na wizara ya kilimo na uvuvi utakaowezesha kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla: Tanzania kuna taasisi nyingi za kifedha kama Bank na taasisi zingine za mikopo. Kama taasisi na mashirika hayo yakifanya kazi kwa ushirikiano na serikali kupitia wizara ya kilimo na uvuvi, basi itasaidia kuinua sekta hii muhimu ya uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.
Sambamaba na hilo,Taasisi hizo za kifedha ziweke utaratibu rahisi na wenye mashariti nafuiu kwa wavuvi na wafanyabiashara wa bidhaa za viumbe maji kwa kuwapataia mikopo. Hii itawapa nafasi wavuvi wadogo kuongeza nyenzo za kazi na kuongeza ufanisi katika kazi zao.
Pia mikopo hiyo ijikite katika wadau na wafanyabiashara wadogo wajiimarishe kwa mfumo wa kisasa wa kuanzisha mabwawa au vizimba vya kufugia na kuzalishia viumbe maji ambavyo vina soko kubwa ndani ya nchi na hata nje ya nchi.
Kitengo cha TEHAMA kilichopo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kifanye tafiti za kisayansi juu ya maeneo ya majini ambapo samaki na viumbe maji wengine vinapatikana kwa wingi; Hii itasaidia kwa wavuvi kufanya shughuli zao kwa faida na siyo kupoteza muda na rasilimalio fedha. Pia itachangia kuondoa uvuvi katika maeneo amayo kuna viumbe maji wachache na kuwaruhusu wazaliane ili uvuvi uwe endelevu.
Mwisho kitengo cha habari katika sekta ya uvuvi kiwe imara kuhabarisha na kutoa taarifa muhimu juu ya sekta hii: Kwa wavuvi na wafanya biashara wadogo wa bidhaa za viumbe maji, inakuiwa ngumu kutambua fursa na habari muhimu zihusuzo sekta hii. Kama kitengo cha habari kikiwa kinatoa masoko yapatikanayo nje ya nchi na hali ya hewa kwa wakati na ufanisi, basi itachangia sana katika kukuza uvuvi na uchumi wa buluu kwa ujumla.