Tishio la njaa duniani, inamaana gani kwa tanzania?
Misukosuko na Janga la Njaa
DUNIA inatarajiwa kukumbwa na janga la njaa kwa mwaka 2023 huku ikitajwa kuwa ni janga mbaya zaidi la njaa kuwahi kutokea duniani kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Chakula Duniani ( WFP ). Mapigano, mdororo wa uchumi, hali ya hewa na kupanda kwa bei za mbolea zimetajwa kuwa sababu zitakazochangia janga hilo la njaa.
Nchi nyingi za Afrika zimeathiriwa na mdororo wa uchumi uliotokana na janga la ‘Corona’ pamoja na vita ya Urusi na Ukraine. Hili ni kutokana na utegemezi mkubwa wa nchi za Kiafrika kwenye uagizaji na usafirishaji bidhaa za gesi na mafuta nje ya nchi, utegemezi kwenye sekta ya utalii sambamba na uagizaji wa mbolea.
Serikali ya Tanzania Imejipanga?
Itakumbukwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan aliweka wazi juu ya tishio la janga la njaa duniani huku akieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali kukabiliana na janga hilo. Ongezeko la mara tatu ya bajeti ya Wizara ya Kilimo ikijikita kwenye umwagiliaji, mafunzo ya ugani, vifaa vya kilimo na ruzuku ya mbolea kwa wakulima ni moja ya mkakati Madhubuti uliowekwa kupambana na janga la njaa.
Sambamba na hilo Rais Samia amekuwa akifungua maghala kwenye mikoa mbalimbali ili mazao yatakayovunwa yabaki kwenye mikoa husika ili janga la njaa litakapotokea liweze kudhibitiwa kirahisi kwenye maeneo husika. Rais Samia aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kumi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wanawake (CCM) ngazi ya Taifa (UWT) uliofanyika Jijini Dodoma.
Nini Kinakwamisha Juhudi?
Utacheka kusikia Mtanzania mfanyabiashara wa mbolea amechakachua mbolea za ruzuku na kuwauzia wakulima mbolea zisizokuwa na ubora na zisizofaa kabisa. Hii ni changamoto kubwa ambayo inaweza kukwamisha juhudi za serikali kufikisha mbolea zilizohakikiwa na zenye matokeo chanya kwa wakulima. Itakumbukwa, Jeshi la Polisi Mkoani Njombe liliwakamata watu kumi kwa tuhuma za kufungasha mbolea feki kisha kuwauzia wakulima mkoani humo.
Mbolea feki zinakwenda kupunguza uzalishaji na kuua ubora wa mazao ya wakulima, ambayo hayatofaa kwenye matumizi ya binadamu na hata kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya biashara hasa kwenye mataifa ya Afrika yaliyoingia kwenye mkataba wa eneo huru la biashara.
Elimu ndogo ya ardhi kwa baadhi ya wananchi ni changamoto itakayokwamisha uzalisha wa mazao kwa wingi. Hii ni kusema kuwa katika baadhi ya maeneo wananchi wamekuwa wakiweka makazi na kufanya shuguli za kilimo kwenye maeneo ambayo hayaruhusiwi kisheria kufanya hivyo. Hii inapelekea kuhamishwa na serikali au wawekezaji wenye ardhi husika jambo linaloleta mdororo wa uzalishaji katika kilimo kwani wananchi wanalazimika kuachana na mashamba yao na kuhamia kwenye maeneo sahihi kwa ajili ya makazi na kilimo. Hii inapelekea uzalishaji kuwa mdogo hivyo mazao yanayopatikana hayatoshelezi kwa ajili ya chakula na usafirishaji wa chakula nje ya nchi kwa ajili ya biashara. Mfano uamuzi wa  Baraza la Mawaziri kuhusu mgogoro wa eneo linalodaiwa kuwemo katika bonde la Ihefu wilayani Mbarali ambapo vijiji vitano vilifutwa.
Umilikishaji wa mali kihalali kwa utoaji wa hati kwa haraka, ili kuepuka migogoro na kusaidia uendelezaji wa ardhi. Ardhi isiyo na mmiliki haiwezi kutunzwa, na hata kuzalisha ipasavyo na kuwafanya wakulima wengi kufanya kilimo cha mazao kwa ajili ya kula tu na sio biashara jambo ambalo linashusha uzalishaji kwa kiwango kikubwa kwa ajili ya biashara nje ya nchi.
Hali ya hewa ikihusisha upungufu wa mvua kwenye baadhi ya mikoa na mvua kubwa zisizo za kawaida zinasosababisha mafuriko ni moja ya changamoto kubwa inayokwamisha uzalishaji wa wingi wa mazao ya chakula. Hii ni kusema mvua zisizotabirika zimekuwa zikiharibu mazao hivyo upatikanaji wa mazao bora ya chakula cha ndani ya nchi na ziada kwa ajili ya kuuza nje ya nchi kuwa ni mdogo.
Tunaweza kuwa na Ziada ya Chakula ?
Tanzania ni moja ya nchi chache duniani yenye maeneo yenye rutuba yanayoruhusu kilimo cha vipindi vyote, lakini pia Tanzania ni moja ya nchi wanachama kwenye mkataba wa eneo huru la biashara. Hivyo kukiwa na uzalishaji mkubwa utakaotosheleza upatikanaji wa chakula nchini na ziada basi itakuwa ni fursa kubwa ya biashara kwa nchi zingine za africa zitakazokuwa na upungufu wa chakula kutokana na uzalishaji mdogo na sababu zingine. Watu zaidi ya Bilion 1.4 waliopo Africa wanaweza kunufaika na mazao yanayozalishwa na wakulima nchini Tanzania na kuweza kuwakamua kutoka kwenye umaskini mkubwa.
Kuna Cha Kufanya
Amani, vyanzo vya maji, ardhi yenye rutuba na juhudi za serikali kwenye kilimo ni sababu kubwa zinazowezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kutosha wa kuzalisha mazao kwa wingi yatakayotosheleza chakula cha ndani ya nchi na ziada kwa ajili ya kulisha Afrika nzima.
Matokeo ya Sensa ya kilimo ya mwaka 2019/20 yanaonesha kuwa kati ya kaya 12,007,839 zilizopo Tanzania bara na Zanzibar jumla ya kaya 7,837,405 (asilimia 65.3 tu) zinajihusisha na shughuli za kilimo. Hii ni kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ( NBS ). Bado kuna hitaji la kaya nyingi kushiriki kwenye kilimo.
Â
Serikali haina budi kufanya uhakiki na udhibiti wa wafanyabishara wa mbolea wanaochakachukua mbolea na kuwauzia wakulima mbolea zisizofaa na zisizo na tija. Hawa ni kama wauaji wa Taifa na dunia. Tunawezaje kumvumilia mtu anayezolotesha uzalishaji wa mazao ya chakula ili tukabiliane na janga la njaa? Haiwezekani.
Sheria lazima ziwe kali juu ya wafanyabiashara na watu wote kuhujumu juhudi zinazofanywa na serikali ya Tanzania kupambana na janga la njaa litakaloikumba dunia.
Wizara ya Kilimo haina budi kueneza elimu juu ya mbolea sahihi zinazofaa kutumika kwenye uzalishaji wa mazao husika. Hapa lazima wakulima wajue nembo na alama zitakazowawezesha kutofautisha mbolea bandia na mbolea sahihi. Hii itawawezesha wakulima kutoa taarifa kwa vyombo husika juu ya upatikanaji na uuzwaji wa mbolea zilizoisha muda na zisizofaa kwenye kilimo.
Tunawezaje kumvumilia mtu anayezorotesha uzalishaji wa mazao ya chakula ili tukabiliane na janga la njaa? Haiwezekani.
Â
Kuna haja ya kuweka mikakati ya kuwa na kilimo cha umwagiliaji hasa maeneo ya vijijini kwa kuchimba mabwawa na visima vikubwa vitakavyokuwa na maji ya kutosha ili yaweze kutumika wakati wa ukame na mvua zisizotabirika.
Wizara ya ardhi iwe mstari wa mbele kueneza elimu juu ya umiliki wa ardhi na kuainisha maeneo yasiyoruhusiwa kwa ajili ya makazi na shughuli za uchumi kama kilimo. Hii itapunguza kuhamahama kwa wakulima kwa kupisha maeneo ya wawekezaji na maeneo yanayomilikiwa na serikali hivyo kuleta matokeo chanya kwa wakulima kuwa na muda mwingi wa uzalishaji wa mazao ya chakula.
Pia katika juhudi hizi za mapambano juu ya janga la njaa litakaloikumba dunia lazima viongozi wa serikali za mtaa na vijiji washirikishwe kikamilifu. Hii ni kusema viongozi hawa ndiyo wapo karibu na maeneo ya wakulima hivyo basi kama wakieleweshwa juu ya hatari ya njaa itakayoikumba dunia basi watashiriki kikamilifu kuhakikisha mazingira wezeshi kwa wakulima.
Mfano watahakikisha ulinzi kwa wakulima muda wote ili wafanye uzalishaji wao kwa amani na uhuru kwa kuzuia migogoro na kuzuia matumizi yasiyofaa ya mazao.
Kama jitihada hizi zikifanyika kikamilifu basi kutakuwa na chakula cha kutosha nchini na ziada ya mazao ya kusafirisha nje ya nchi kwa ajili ya biashara hivyo Tanzania itanufaika kwa kiwango kikubwa katika eneo huru la biashara Afrika kwa nchi wanachama.
Bakari Mahundu amejitambulisha kama mdau Mwandishi wa habari na Mtafiti wa masula ya vijana Tanzania. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia bakarimahundu8@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa Liberty Sparks. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia info@libertysparks.org kwa ufafanuzi zaidi.