Namna Serikali Inavyoweza Kutatua Changamoto ya Mafuta ya Kula.
Kulingana na takwimu za sasa; Idadi ya Watanzania ni zaidi ya milioni 55, huku zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania hawa ni Wakulima, ambao wengi wao wanaishi maeneo ya Vijijini na hufanya shughuli ya kilimo kwa ajili ya kujikimu huku wachache wao wakifanya kilimo cha biashara kwa kuongezea thamani mazao yao!.
Kilimo ni moja ya sekta muhimu zaidi Afrika Mashariki. Tanzania kumebarikiwa eneo kubwa la ardhi, lenye hekari 362000, ambalo linafaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo Mahindi, Ufuta , Pamba pamoja na Alizeti. Kulingana na Benk ya Tanzania (BOT) 2018, sekta ya kilimo inachangia asilimia 30 ya pato la Taifa na kwa ukubwa huo sekta hii ya kilimo ni mara tatu ya Sekta ya biashara, kwa asilimia 11, madini kwa asilimia 4.8 na uzalishaji na viwanda kwa asilimia 5.5.
Tanzania imekuwa na tatizo la upungufu wa mafuta ya kula kwa kiwango kikubwa, kwa mwaka 2021 pekee , mafuta ya kula katika jiji la Dar es saalam, yalipanda bei na kufikia kati ya Sh. 26,000 hadi 29,000 kutoka bei ya awali ya 20,000. Huku lita moja ikiuzwa mpaka Sh. 5,000 tofauti na bei ilioyokuwapo ya Sh. 3500 kabla ya bidhaa hiyo haijapanda!.
Kulingana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mh. Kasimu Majaliwa alipozungumza mkoani Singida Juni 13, mwaka huu; Uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ni mdogo ambapo ni tani 290,000 tu ambazo uzalishwa nchini, kiasi hicho ni sawa na asilimia 45 ya mahitaji ya mafuta ya kula ambayo ni tani 650,000 kwa mwaka. Huku Serikali ikiagiza tani zipatazo 400,000 kufidia upungungufu wa mafuta ya kula na hugharimu zaidi ya Shilingi bilioni 474 kwa mwaka , kwa takwimu za sasa!.
Hivyo basi, biashara ya mafuta ya kula na kilimo cha alizeti ni fursa adhimu mno kwa watanzania na wawekezaji kutoka nje kama serikali na taasisi husika zikiweka mikakati madhubuti na imara kwa wakulima, wawekezaji na wafanyabiashara wa mafuta ya kula wa nje na ndani ya nchi:
Serikali kuweka utaratibu rahisi na nafuu kwa wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza nchini; Kama serikali ya Tanzania, itahakikisha mfumo na utaratibu wa uhakika na rahisi unaowahakikishia wawekezaji kuja nchini kuwekeza katika mashamba ya alizeti pamoja na viwanda vya mafuta, basi kutakuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta nchini. Hii itasaidia kuondoa hasara inayopata serikali kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi na kujiongezea mapato yatokanayo na kodi katika bidhaa na viwanda hivyo vya mafuta nchini.
Sambamba na hilo, Serikali na wizara husika iandae zihara za kitalii na kuruhusu wamiliki wa viwanda vya mafuta ya kula na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi; Kama wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya mafuta kutoka nje watapata nafasi ya kuja kutembelea nchini basi wataona fursa kubwa zilizopo nchini juu ya kilimo cha alizeti na biashara ya mafuta ya kula. Hii itakuwa rahisi kushawishika na kuja kuwekeza nchini katika uchakataji na uzalishaji wa mafuta ya kula, hivyo kuongeza kiwango cha upatikanaji wa mafuta haya na kuipunguzia hasara serikali kwa kiwangio kikubwa kutokana na kuagiza mafuta hayo nje ya nchi kila mwaka.
Serikali na taasisi husika kuweka punguzo la ushuru ama kuondoa kabisa ushuru wa mashine za kuchakatia mafuta ya kula kwa wawekezaji wa ndani ama wazawa; Kwa kiwango kikubwa, wazalishaji wa mafuta ya alizeti hawana uwezo wa kumudu gharama za kumiliki mashine za kisasa za kukamulia mafuta, hivyo kusababaisha hasara kubwa inayotokana na upotevu wa mafuta wakati wa uchakataji na usindikaji kutokana na vifaa duni wanavyotumia. Kama serikali itaweka utaratibu wa kuwapunguzia kodi ama kuondoa kabisa ushuru wa mashine zitokazo nje kwa ajili ya uchakataji wa mafuta ya kula, basi itawezesha upatikanaji wa mafuta kwa kiwango kikubwa na kwa bei rafiki. Na hivyo kuiepusha serikali  gharama ya kuagiza mafuta hayo nje ya nchi.
Sambamba na hilo Serikali kupitia Benki kuu inapaswa kupunguza riba za mikopo kwa wakulima ili kuwawezesha wakulima wadogowadogo wa zao la alizeti waweze kupata mikopo ya riba nafuu zaidi na utaalamu wa bure katika mashamba yao; Hasara inayoingia serikali kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi kupitia fedha za walipa kodi kila mwaka ni ya kutisha, na inazuia ukuaji wa maendeleo ya Taifa letu. Kama Selikari kupitia benki kuu kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi nchini zikitoa mikopo kwa wakulima na wawekezaji wadogowadogo , wakati na wakubwa ambao ni wazawa , basi kutakuwa na ongezeko kubwa la mafuta ya kula nchini na kusaidia upatikanajai wa bidhaa hiyo muhimu nchini na kupata nafasi ya kuuza mafuta hayo nje ya nchi. Hapana shaka Tanzania kuna wataalamu wa kilimo wanaoweza kutoa elimu madhubuti kwa wakulima hawa na kuwaongoza katika namna bora ya uandaaji, upandaji, uvunajai na uchakataji wa bidhaa hiyo na kuongeza thamani.
Pia, Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi mbalimbali za kilimo nchini, zifanye tafiti juu ya mikoa mingine tofauti ambayo inaweza kuzalisha zao la alizeti; Hapa kuna ulazima wa wataalamu wa mambo ya ardhi na udongo, kufanya tafiti juu ya mikoa mingine tofauti ambayo inawezesha kustawisha zao la alizeti na sio kutegemea mikoa kadhaa ambayo imeonekana kufanya vizuri katika zao hilo kama, Singida. Hivyo basi, mikoa kama Mtwara na Lindi ambayo imejikita zaidi katika mazao ya Korosho na ufuta , kuna umuhimu wa kuruhusu taasisi binafsi zenye wataalamu kufanya tafiti juu ya aina ya mbegu za alizeti zinazoweza kulimwa katika mikoa hiyo. Hii itachangia kuongezeka kwa mikoa inayozalisha zao hilo na kupelekea kuongezeka kwa mafuta ya kula nchini, hivyo kuepusha serikali hasara kubwa ya zaidi ya Shilingi bilioni 474 katika kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi!.
Mwisho, Kuna ulazima wa Serikali kuruhusu tafiti kufanyika ili kupatikana kwa zao mbadala la alizeti ambalo linaweza kuzalisha mafuta kwa wingi; Bila shaka Tanzania kuna mazao mengi yanayoweza kuzalisha mafuta ya kula ukiachana na alizeti. Mazao kama: Michikichi na karanga ambazo zinaweza kuchakatwa na kuzalisha mafuta kwa kiwango kikubwa. Kama hatutotegemea mazao ya alizeti pekee katika uzalishaji wa mafuta na kuongeza mazao mengine ya kimkakati katika uzalishaji wa mafuta ya kula,basi kutakuwa na uzalishaji mwingi wa mafuta ya kula na kuipunguzia serikali hasara kubwa ianayoingia kila mwaka ya kuagiza bidhaa ya mafuta ya kula nje ya nchi kila mwaka.