Umuhimu wa bandari katika uchumi na maendeleo ya nchi.
Miezi michache iliyopita waziri mkuu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa alifanya ziara katika bandari ya Dar es salaam na kuzungumza mambo mbalimbli ikiwa ni pamoja na kuwataka TRA kufanya kazi kubwa maeneo ya bandari, Lakini pia aligusia mfumo unaotumika unavyoharibu kazi.
Nchi zilizoendelea zinatazama bandari kama chanzo muhimu cha kipato na maendeleo ya nchi wakati bandari kubwa ulimwenguni zinapakia na kupakua hadi tani millioni 744 za shehena kwa mwaka.
Tanzania tumebarikiwa kuwa na bandari katika mwambao wa bahari ya hindi inayohudumia nchi jirani zenye bandari na zisizo na bandari kama vile Msumbiji, Burundi, Rwanda, Malawi, Congo na Zambia ambao wanatumia kupakia na kupakua mizigo kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni na kupelekea bandari ya Dar es salaam kuwa ni chanzo kikubwa na mapato na kukua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.
Miaka ya hivi karibuni kulikuwa na migogoro ya hapa na pale kati ya nchi zinazotumia bandari hiyo kwa nyakati tofauti ikiwemo Zambia na DRC Congo na changamoto kubwa ikiwa ni urasimu katika usafirishaji wa mizigo inayopitia bandari ya Dar es salaam kwenda katika nchi hizo kitu ambacho hakikuleta taswira nzuri kibiashara na kiuchumi baina ya nchi hizi kwa wakati ambao nchi hizi zinapambana kujijenga kiuchumi kupitia ushirikiano wao na sio migogoro.
Bandari ya Dar es salaam kwasasa inabeba chini ya tani million 20 ni kiasi cha kawaida ukilinganisha na idadi ya nchi zinazotegemea bandari hiyo, hivyo serikali inahaja ya kuangalia na kuongeza eneo ili kuongeza kiasi cha mizigo inayoshushwa na kupakiwa hadi kufikia zaidi ya millioni 30 ambazo zitakidhi mahitaji ya nchi zote zinazotumia bandari hiyo.
Jambo mojawapo linaloonesha ufanisi wa bandari ni ubora wa huduma zinazotolewa na bandari husika ikiwa ni pamoja na meli kuhudumiwa kwa muda mfupi zaidi bila kusababisha hasara kwa wenye meli na wafanyabiashara ni muhimu kulitazama hili kwasababu ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya viwanda na biashara.
Uwepo wa bandari hii ni fursa kubwa sana kiuchumi na uwepo wa soko huria huleta ushindani wa kibiashara, linahitaji huduma zenye uhakika na haraka ili kukidhi ubora wa kimataifa kwa kuzingatia namna bora ya uendeshaji wa bandari, ubora wa miundombinu na matumizi ya teknolojia ya kisasa.
Nchi mbali mbali barani Afrika zinafaidika kwa maendeleo kutokana na uwepo wa bandari na kutulia mkazo katika sekta hiyo, nchi kama Afrika kusini inaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa hatua waliopiga kiuchumi kutokana na kulitazama suala la uwepo wa bandari kama sehemu na kichocheo cha kukua kwa uchumi wa nchi kupitia sera yao ya ‘operation phakisa’ iliyozinduliwa rasmi mwaka 2014 ukiwa ni mpango wa makusudi wa kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mpango wa taifa wa maendeleo ifikapo mwaka 2030.
Lakini pia kwa nchi kama Mauritius ilichukua hatua za makusudi kuimarisha uchumi wao kwa kutazama uchumi wa bahari kama sehemu muhimu ya kuboresha na moja ya nguzo ya uchumi wa nchi na kuwasaidia kufikia malengo yao ya kimkakati ya kiuchumi kukua hadi kufikia uchumi wa juu ambao walifanikiwa kuufikia huko mapema mwaka 2020, kwasasa Mauritius wanategemea mchango wa uchumi kutokana na bahari kufikia hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2025.
Kama nchi ni muhimu kugeukia katika uchumi wa bluu na kutazama fursa za kimaendeleo na kutilia mkazo na kuiwekea kipaumbele kama ilivyo kwa sera ya kilimo na viwanda kwa miaka ya hivi karibuni. Rasilimali watu wenye ujuzi, na uzoefu wa kutosha, weledi, juhudi, uadilifu inaweza kuleta mabadiriko makubwa ya kimaendeleo na uendeshaji wa bandari.
Malengo ya maendeleo endelevu kwa jamii na nchi inapaswa kuwekeza katika elimu zaidi ili kupata rasilimali watu, uchumi wa blue ni fursa na chachu ya maendeleo kwasababu unatengeneza ajira zenye staha, ukuaji wa viwanda na uwekezaji, biashara za kimataifa na fursa zingine mbalimbali.
Serikali inatakiwa kuangalia sheria katika eneo hili haipaswi kuweka sheria kandamizi kwa watumiaji wa bandari ya Dar es salaam zikiwepo nchi jirani kama Congo na Zambia ambazo zinategemea zaidi kuingiza mizigo yao kupitia bandari ya Dar es salaam kama taifa linanufaka kwa kuingiza kipato na maendeleo ya miundo mbinu inayotumiaka kusafirisha mizigo.
Lakini pia kuwe na ushirikiano mzuri kati ya sekta za uma na sekta za binafsi ili kusaidiana katika maendeleo ya nchi kama kuboresha miundombinu ya bandari ili kuwa na uwezo wa kubeba zaidi ya tani millioni 30 za mzigo ili kukidhi mahitaji na matumizi ya bandari hiyo kwa nchi za Afrika mashariki na kati.