Safari za Jonathan Gullible
Misingi ya Mwongozo
Falsafa yangu imejengwa juu ya msingi wa umiliki binafsi. Unamiliki maisha yako. Kukana jambo hili ni kumaanisha kwamba mtu mwingine ana uamuzi mkubwa zaidi juu ya maisha yako kuliko ulionao. Hakuna mtu mwingine, au kundi la watu, anayemiliki maisha yako wala wewe humiliki maisha ya wengine.
Unaishi na upo katika nyakati: wakati ujao, wakati uliopo, na wakati uliopita. Jambo hili ni dhahiri katika maisha, uhuru, na katika yote yatokanayo na maisha na uhuru wako. Zoezi la kufanya chaguzi juu ya maisha na uhuru ni ustawi wako. Kupoteza maisha yako ni kupoteza wakati wako ujao. Kupoteza uhuru wako ni kupoteza wakati wako uliopo. Na kupoteza yote yatokanayo na maisha na uhuru wako ni kupoteza sehemu ya wakati wako uliopita uliozaa mambo hayo.
Yote yatokanayo na maisha na uhuru wako ni mali yako. Mali ni tunda la nguvukazi yako, ni zao la muda, nguvu, na vipaji vyako. Ni ile sehemu ya asili yako unayoigeuza kwa matumizi yenye manufaa. Na ni mali za wengine ambazo unapewa kupitia mabadilishano au biashara ya hiyari na ridhaa ya pande zote mbili. Watu wawili wanaobadilishana au kuuziana mali kwa hiyari huneemeka wote wawili la sivyo wasingefanya hivyo. Ni wao peke yao wanaoweza kwa haki kabisa kufanya uamuzi huo kwa ajili yao wenyewe.
Kuna nyakati baadhi ya watu hutumia nguvu au hila kuchukua maisha, uhuru au mali kutoka kwa wengine bila ya ridhaa itokanayo na utashi au hiyari yao. Kwa kawaida, matumizi ya nguvu ili kuchukua maisha ni mauaji, kuchukua uhuru ni utumwa, na kuchukua mali ni wizi. Inabakia kuwa hivyo bila kujali haya matendo yanafanywa na mtu mmoja peke yake, yanafanywa na wengi dhidi ya wachache, au hata kama yanafanywa na maofisa wa serikali wenye suti na vyeo vya kuvutia.
Unayo haki ya kulinda maisha yako, uhuru, na mali unazomiliki ambazo zimepatikana kihalali. Unaweza kihalali kabisa kuomba wengine wasaidie kukulinda. Hauna haki ya kuanzisha matumizi ya nguvu dhidi ya maisha, uhuru, au mali wanazomiliki wengine. Kwa maana hiyo, hauna haki ya kutuma mtu au watu fulani kuanzisha matumizi ya nguvu dhidi ya wengine kwa niaba yako.
Unayo haki ya kutafuta viongozi kwa ajili yako mwenyewe, lakini hauna haki ya kulazimisha utawala wako juu ya wengine. Haijalishi ni jinsi gani maofisa wa serikali huchaguliwa, hawana haki au stahili ambazo ni juu zaidi kuliko zile za mtu mwingine yeyote. Huwezi kuwapa haki zozote ambazo wewe mwenyewe huna. Bila ya kujali vyeo vya kufikirika, maofisa wa serikali hawana haki ya kuua, kutumikisha, au kuiba. Huwezi kuwapa haki zozote ambazo wewe mwenyewe huna.
Kwa kuwa unamiliki maisha yako, una wajibu juu ya maisha yako. Unajichagulia malengo yako na maadili yako mwenyewe. Haujakodisha maisha yako kutoka kwa wengine ambao wanadai utii wako. Wala siyo mtumwa wa wengine ambao wanadai sadaka yako.
Unajiwekea malengo yako mwenyewe kulingana na maadili yako mwenyewe. Yote mawili; kufanikiwa na kutofanikiwa ni kichocheo muhimu cha kujifunza na kukua. Matendo yako kwa niaba ya wengine, au matendo yao kwa niaba yako, yanakuwa halali pale tu pale yanapotokana na ridhaa ya hiyari, kutoka pande zote husika. Kwa maana tunu za “wema na adili” huwa pale tu ambapo kuna uhuru wa kuchagua.
Huu ndiyo msingi wa jamii huru ya kweli. Siyo tu msingi unaofanya kazi vizuri zaidi na wenye kuzingiatia ubinadamu katika matendo ya watu; bali ni msingi wenye kufuata maadili.
Matatizo yanayoibuka kutokana na matumizi ya nguvu ya serikali yana utatuzi wake. Utatuzi wake ni watu wa dunia hii kuacha kuwaomba maofisa wa serikali kutumia nguvu kwa niaba yao. Uovu hauibuki kutoka kwa watu waovu pekee, bali kutoka kwa watu wema pia ambao wanavumilia matumizi haya ya nguvu kama njia ya kujipatia manufaa yao wenyewe. Kupitia utaratibu huu, watu wema wamewapa nguvu waovu katika vipindi vyote vya historia ya mwanadamu.
Kujiamini katika jamii huru ni kujikita kwenye mchakato wa ugunduzi katika thamani ya soko badala ya kujikita kwenye dira au lengo fulani lililowekwa tayari. Kutumia nguvu za dola kulazimisha dira kwa wengine ni uzembe wa ‘kisomi’ na mara nyingi huishia katika matokeo potofu kinyume na matarajio. Kuwa na jamii huru kunahitaji ujasiri wa kufikiri, kuongea, na kutenda – hasa pale ambapo ni rahisi zaidi kutofanya chochote.