Kahawa: Bidhaa ya kwanza kuipeleka AfCFTA. Tunaenda Kumuuzia Nani?
“Tayari tuna bidhaa ya kwanza tutakayoiuza nje, na bidhaa hiyo ni kahawa…hatotuoiuza ghafi bali tutauza kama bidhaa iliokamilika”. Alinukuliwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mh. Dk Ashatu Kijaji akiwaeleza wajumbe wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) juu ya uamuzi wa serikali kuisajili kahawa kama bidhaa ya kwanza kutoka Tanzania kwenye soko la biashara la eneo huru barani Afrika (AfCFTA). (Soma: https://allafrica.com/stories/202302140473.html).
Uamuzi huu ulifikiwa baada ya majadiliano ya miezi kadhaa baina ya serikali na wadau mbalimbali juu ya ipi iwe bidhaa ya kwanza kupelekwa kwenye soko la watu zaidi billioni 1.3.
Ikumbukwe Tanzania iliwasilisha uthibitisho wa kukubali uanachama na utekelezwaji wa mkataba huu (AfCFTA) mnamo tarehe 01 Januari 2021, hivyo iliweza kupata muda wa kutafiti na kujiandaa na ushindani pindi soko litakapofunguliwa.
Ukiachilia mbali Korosho na Tumbaku; Kahawa ni bidhaa ya kilimo ya tatu nchini yenye kuchangia pato kubwa ikikadiriwa mwaka 2021/22 kuchangia zaidi ya USD Millioni 142 baada ya mauzo. (Rejea: www.statista.com/statistics/1310392/value-of-agricultural-exports-from-tanzania na Hotuba ya Wizara ya Kilimo 2022/23, Uk 84).
Hali ya Kahawa Nchini (Uzalishaji).
90% ya wazalishaji wa kahawa nchini ni wakulima wadogo wadogo ambao huuza bidhaa zao kwa wafanyabiashara moja kwa moja au kupitia vyama vya ushirika. Serikali imekuwa ikijikita zaidi kwenye kuwawezesha wakulima kwenye elimu na uzalishaji hasa kwenye ugawaji wa miche, mbolea, dawa n.k pia usimamizi wa sera za soko na wataalamu hasa maafisa ugani.
Uzalishaji wa kahawa nchini umezidi kukua mwaka hadi mwaka; mfano mwaka (2017/18) uzalishaji ulikuwa tani 45,245, (2018/19) tani 68,147, (2019/20) tani 60,651, (2020/21) tani 73,027 na mwaka (2021/22) inakadiriwa kufika zaidi ya tani 65,235. Uzalishaji kwa mwaka 2019/20 ulipungua baada ya kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ulioathiri hali ya upatikanaji wa mahitaji ya uzalishaji hasa mbolea, pembejeo n.k ila pia mahitaji ya soko kupungua. (Rejea: Hotuba ya Wizara ya Kilimo 2022/23, Uk 91).
Serikali imekuwa ikiendelea kuweka mkazo kwenye uzalishaji; hasa ikitazamwa katika bajeti ya Wizara ya Kilimo 2022/23 ilitenga kiasi cha TZS Milioni 300 ambazo zingetumika katika uzalishaji na usambazaji wa miche bora 20,000,000 na kununua mashine mbili zenye uwezo wa kukaanga tani 15 za kahawa kwa saa, pia ukarabati wa mashamba, mafunzo ya kilimo bora,
uimarishaji wa masoko ikiwemo kuanzisha minada ya kahawa na kuratibu usimamizi wa mikataba ya ununuzi wa kahawa mfano mkataba wa AfCFTA).
Hali ya Soko la Kahawa
Ethiopia ni nchi ya kwanza barani Afrika na ya tano duniani kwa uzalishaji mkubwa na uuzaji wa kahawa ghafi ikikadiriwa kuuza zaidi ya tani 280,560 ikifuatiwa na Uganda ambayo mwaka 2022 kati 17%-19% ya fedha zote za kigeni zilipatikana kwenye mauzo ya kahawa. Nchi hizi mbili zimekuwa zikifanya biashara zaidi na mataifa kama Italia, Ujerumani, USA, Japan, Ubelgiji na mataifa ya Mashariki ya kati. (Rejea: U.S Foreign Agricultural Service, www.fas.usda.gov/data/ethiopia-coffee-annual-6 na https://www.fas.usda.gov/data/uganda-coffee-annual-6).
Nchini Uganda, serikali imeonekana kujidhatiti kwenye uzalishaji na masoko; Kulingana na Mamlaka ya Maendeleo ya Kahawa nchini Uganda (UCDA), ustawi wa biashara hiyo itahitaji ongezeko la wanunuzi ambapo taasisi hiyo imelenga kupenya zaidi kwenye soko la China na mataifa ya Ulaya. Takwimu za mwaka 2021-2022 zilionesha Uganda ndio nchi pekee iliyowahi kupata kipato kikubwa kitokanacho na mauzo ya Kahawa ndani (ya mwaka mmoja) kwa kuuza bidhaa hiyo kwa thamani ya USD Milioni 862. (Rejea: Investment Monitor: https://www.investmentmonitor.ai/features/can-uganda-become-a-coffee-powerhouse).
Mataifa mengine yaliyojikita kwenye kilimo cha Kahawa barani Afrika ni Ivory Coast, Burundi, Rwanda na Kenya.
Kahawa Afrika? Tunamuuzia Nani?
Kama zilivyo nchi nyingi wazalishaji wa kahawa Afrika, Tanzania pia imekuwa ikiuza kahawa ghafi kwenye mataifa kama Japan, Italia na USA. Hali hii ya uuzaji wa kahawa katika mataifa haya ya nje ndio imepelekea taifa kuendelea kuwekeza zaidi kwenye kilimo hiki. Ripoti ya Tasnia ya Kahawa Tanzania: Mkakati wa Maendeleo 2011-2021, imeeleza kwa kina mpango wa ongezeko la uzalishaji kutoka wastani wa tani 50,000 hadi kufikia tani 100,000 mwaka 2021. Mpango huu kulingana na takwimu zilizooneshwa hapo juu kwa mwaka 2021 ni dhahiri zilishindikana kufikika.
Katika utekelezaji wa mkataba huu, moja ya njia ya kufikiwa malengo haya ni kuongeza mauzo kwenye mataifa washirika ya kibiashara hasa nchi kama Japan ambayo huchangia 15% ya mauzo ya bidhaa hii, Ujerumani, Italia na Ubelgiji (zote zikichangia 10%), huku 25% iliobakia ikipangwa kugawanywa kwenye nchi toauti tofauti hasa Finland na Switzerland.
Kulingana na Jukwaa la Uchumi Duniani, Afrika imekuwa na matumizi madogo ya kahawa ikilinganishwa na mataifa/jumuiya zingine duniani. Ukiachilia mbali taifa la Ethiopia ambao hupendelea kahawa ya “kwao” inayofahamika kama “ Yirgacheffe” ambapo kwa mwaka matumizi ya mtu mmoja ni kg 2.27,
mataifa mengine yamekuwa na utumiaji mdogo. Inakadiriwa nchi ya Algeria ni kg 3.2, Madagascar matumizi ni kg 1, Ivory Coast kg 0.9 kwa mtu mmoja kwa mwaka, huku taifa kama la Brazil matumizi ni kg 6. Ripoti ya Euro Monitor ilielezea mataifa ya Ivory Coast na Uganda ambao ni wazalishaji wakubwa wa kahawa ingawa wananchi wake kwa wingi hutumia kakao na chai badala ya kahawa. Rejea: https://www.weforum.org/agenda/2015/10/which-african-countries-produce-the-most-coffee na https://www.emerald.com/insight/content/doi/10.1108/JHASS-03-2021-0046/full/html)
Kulingana na maelekezo ya Waziri Kijaji, Tanzania inapaswa kupeleka kahawa iliokamilika kama bidhaa na sio ghafi tena. Nchi nyingi za Afrika zimekuwa na utaratibu zinazoathiri uchumi wake kwa kutokuwekeza kwenye uendelezaji wa mnyororo wa bidhaa kwa kuziongezea thamani na kuziuza zikiwa ghafi. Bajeti ya Wizara ya Kilimo Pamoja na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara zinapaswa kuangalia ni kwa namna gani baadhi ya bidhaa tunazozitengeneza ziingizwe kwenye soko la ushindani ziweze kuongeza thamani kwenye uchumi wetu.
Pamoja na hayo, tafiti kubwa zifanyike kwenye chaguzi wa bidhaa kwenye soko la ushindani hasa mkataba wa AfCFTA unaotekelezwa sasa, kwani kwa bidhaa kama kahawa ambayo soko lake kubwa limekuwa kwenye mataifa ya nje, kuiweka kama bidhaa namba moja kwenye ushindani katika soko la AfCFTA inaweza isiwe na tija kwa kuwa sio bidhaa hitajika kwenye soko la Afrika.
Chaguzi ya bidhaa hizi pia zinapaswa kusindikizwa na mpango wa kuzilinda kwenye ushindani kupitia bajeti ya wizara na serikali kuu Pamoja na wataalam wa soko na ushawishi. Kiujumla uwekezaji katika ushindani unapaswa kuzingatiwa.
Tanzania inaweza kuitumia fursa hii ya kuitangaza kahawa katika soko la AfCFTA, ili kupata uwekezaji wa viwanda ndani ya nchi kutokana na sheria ya mkataba ya “Rule of Origin”ambayo inahitaji bidhaa izalishwe ndani ya Afrika. Changamoto ni uwepo wa soko la kuhakikisha uwekezaji huu unalipa kwa mwekezaji na serikali kwa ujumla.
Ni wazi tutatambulisha bidhaa hii katika soko la AfCFTA, Julai 2023 lakini haitoweza kushindana na kuleta tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla.