Mageuzi ya kilimo kupitia gmo: je, ni suluhu ya ukame na biashara ya kilimo afrika?
Januari 1, 2021 yalisainiwa rasmi makubaliano ya utekelezaji wa mkataba wa eneo huru la biashara barani Afrika (AfCFTA). Shabaha yake ni kukuza mashirikiano ya kibiashara baina ya nchi washirika kutoka 18% (sasa) hadi kufikia 52.3% kwa kuondoa ushuru wa forodha pamoja na kupunguza vizuizi visivyo na ushuru kwa bidhaa zaidi ya 60,000. Hatua hii inatarajiwa kukuza uchumi wa Afrika kufikia USD 29 trilioni ifikapo mwaka 2050.
Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) linaitaja Afrika, kama jumuiya yenye mchango mdogo zaidi duniani kwenye biashara ikichangia 2% tu. Kwa sasa jumla la pato zima la bara hilo ni USD Trilioni 3.4, hivyo kutekelezwa kwa mkataba huu kutaifanya pato likuwe kwa 7% kila mwaka. Kulingana na mapendekezo ya Kamisheni ya Uchumi wa Afrika (ECA), inaeleza moja ya mpango utakaofanikisha malengo haya kutimia ni uzidishaji wa bidhaa za kilimo.
Ikumbukwe; Mwaka 2003 ulisainiwa Mkataba wa Azimio la Maputo uliozitaka nchi wanachama wa AU kutenga 10% ya bajeti kuu ya matumizi kila mwaka kwa ajili ya Kilimo. Nchi nyingi zimekuwa zikitenga kati ya 2-3%, hivyo kuifanya sekta ya kilimo kuendelea kudumaa. Mfano, mwaka 2020, ni nchi nne tu zikiwemo Malawi, Lesotho, Ethiopia na Benin) zilizotenga bajeti yake kwa zaidi ya 10% kwenye kilimo
Hali hii inapelekea usalama wa chakula Afrika kuendelea kupungua. Ripoti ya Shirika la Biashara na Maendeleo Duniani (UNCTAD), ilieleza kuwa kati ya mwaka 2016-2018; 85% (thamani ya USD Bilioni 35 kwa mwaka) ya matumizi yote ya chakula Afrika iliagizwa kutoka Mataifa ya nje. Hivyo inakadiriwa kufikia mwaka 2025, uingizaji wa chakula kutoka nje utaongezeka na kufika USD Bilioni 110 kwa mwaka.
Ukiachilia mbali kiwango kidogo kinachotengwa kwenye bajeti ya Kilimo kwenye nchi nyingi za Afrika, pia kumekuwa na sababu mbalimbali zinazopelekea uzalishaji wa mazao ya kilimo kudorora. Sababu kama Matumizi duni ya teknolojia, Mabadiliko ya tabia nchi, elimu ya mabadiliko ya uzalishaji wa mazao, kukosekana kwa mnyororo wa uthaminishaji wa mazao ya kilimo n.k zimekuwa zikichochea sekta hii kushindwa kukua kwa kasi. Shirika la chakula Dunia (WFP), inaeleza kwa sasa watu Milioni 346 barani Afrika wanakabiliwa na upungufu wa chakula, zaidi chanzo ikiwa ni ukame.
Athari ya Ukame na uzalishaji mdogo wa Chakula unatazamiwa kuathiri hali ya Uchumi Afrika hasa kwenye ustawi wa watu kwenye lishe na gharama za upatikanaji wa bidhaa hizo, pia hali hiyo inatazamwa kutaathiri biashara ya mazao ya kilimo baina ya nchi washirika wa AfCFTA.
Mbegu za Uhandisi Jeni (GMO) ni Suluhisho la Ukame; Chakula na Biashara barani Afrika?
Tarehe 3, Oktoba 2022 serikali ya Kenya iliondoa katazo la Utafiti, Uzalishaji na Uingizaji wa mazao yanayotokana na mbegu za GMO. Katazo hili lililodumu kwa miaka 10, liliondolewa baada ya kuonekana kukua kwa ukame uliopelekea upungufu mkubwa wa chakula na maji. Ifahamike kuwa matumizi ya mbegu za GMO kwenye kilimo yameidhinishwa kwenye nchi 8 tu Afrika.
Kulingana na serikali ya Kenya; matumizi ya mbegu hizo yatapelekea ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula hasa ikitazamiwa mbegu hizi kuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili ukame, kupambana na wadudu na pia kuongeza uzalishaji.
Kuchelea kwa mataifa mengi barani Afrika Pamoja na changamoto zake za chakula kupokea teknolojia hii; imechagizwa na maswali mengi ambayo baadhi ya tafiti zilizofanywa zimeonesha mbegu hizi kutokuwa suluhisho la changamoto ya uzalishaji wa mazao (hayo) pia kuonekana kuwa na athari kwenye afya ya binadamu na wanyama.
Waziri wa Kilimo nchini Tanzania, Ndugu aliwahi kunukuliwa na gazeti moja la kila wiki akilinganisha uzalishaji wa pamba itokanayo na mbegu za GMO, ikionekana huzalisha 850 kg huku mbegu za kawaida (Hybrid and Open Pollinated) hukizalisha zaidi ya Tani 1.2-1.75 kwa ekari moja. Mpishano wa uzalishaji huo umeonekana pia kwenye mazao mengine, hivyo kuifanya mbegu hii kutokuonekana jawabu la uzalishaji mdogo.
National Center for Biotechnology Information ilielezea matumizi ya kemikali ya glyphosate ambayo hutumika kwenye utengenezaji wa mbolea ya mbegu ya GMO. Kemikali hiyo ilionekana kuleta athari kwenye viumbe ndani ya udongo na hivyo ili viumbe hivyo visipatwe na madhara hayo, vitahitajika vibadilishiwe uhandisi wa maumbile (GMO genetic engineering) ili viweze kupambana na mazingira. Hali hii itapelekea utegemezi wa teknolojia katika uzalishaji wa chakula ila pia kuharibu ikolojia asili ya viumbe hai.
Matumizi ya mbegu za GMO pia yameonekana kuathiri mazao yaliyo karibu, hasa ikizingatiwa kuwa mimea itokanayo na GMO ni mimea vamizi (invasive species) na hivyo inapotokea uchavishaji (Cross Pollination), mimea mingine inakuwa kwenye hatari ya kuharibika. Kwa hali hiyo, mbegu hizi zinaonekana kuweza kuathiri mimea na mazao mengine yasiyo na maumbile ya GMO, hivyo inalazimisha mimea yote kutengenezwa kwa mfanano wa maumbile ya GMO ili iweze kuishi. Jambo hili limeonekana kutishia uasili wa viumbe hai.
Taasisi ya Afya ya“The Lancet” ya Nchini Uingereza, ilifanya tafiti ya kuhusu vyakula vilivyozalishwa na mbegu ya GMO, tafiti hiyo ilionesha kuwa, mfano “Kiazi” ambacho kiliwekewa Bacillus Thuringiesis kama kemikali itakayotumika kukisaidia kupambana na wadudu.
Tafiti hiyo ilionesha endapo kama mwanadamu atakitumia atakuwa yupo hatarini kuathiriwa kiafya hasa uwezo wake wa kupambana na magonjwa, ukuaji wa chombo (organ), pamoja na mfumo wake wa mmengenyo wa chakula.
Pia kumekuwa na mkingamo wa umiliki wa teknolojia hii, hasa ikizingatiwa kuwa utengenezaji wa mbegu hizi hufanywa na taasisi binafsi; hali hii imeonekana italazimisha mataifa mengi kukabidhi haki ya upatikanaji wa chakula wa wananchi wao kwa taasisi binafsi. Suala hili linatazamwa kuathiri uhuru wa mwanadamu kwenye upatikanaji wa chakula.
Yapi Matokeo na Nini Kifanyike?
Mataifa mengi barani Afrika yameonekana kutokuwa tayari kupokea teknolojia hii. Hali hii itapelekea mataifa yaliyo idhinisha matumizi ya teknolojia hii kutokuwa na uwezo wa kuuza bidhaa hizo nje ya mipaka yao. Hatua hii itaathiri kwa kiwango kikubwa mashirikiano ya kibiashara ya chakula na mazao baina ya nchi washirika wa mkataba wa AfCFTA. Hatua hii inaweza kuwezesha mataifa hayo kujilisha pasipo kuwa msaada wa mataifa mengine.
Kwa kuwa shabaha ya mkataba wa AfCFTA ni kuondoa ushuru wa forodha ili kurahisisha muingiliano wa kibiashara na kuchagiza uchumi kukua. Mgawanyiko huu wa uzalishaji na ununuaji wa bidhaa ndani ya jumuiya ya nchi washirika vitachelewesha au kusababisha lengo hili lisifikiwe. Nchi za Afrika zinapaswa kuweka mkazo kwenye sera za kilimo na mnyororo wa bidhaa za kilimo.
Mataifa yenye hatari ya kupata ukame mara kwa mara yanapaswa kuweka mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo yasiyo na ukame na kujikita zaidi kwenye kilimo cha mazao yanayohimili ukame ambayo pia yanaweza kuzalishwa kwa ziada na kuuzwa katika mataifa mengine. Mataifa haya yanapaswa kurudi na kutekeleza makubaliano ya Maputo kwani tafiti zimeonesha ustawi wa sekta ya kilimo baada ya kutenga bajeti ambayo itawezesha kufanyika kwa tafiti, usimamizi wa sera, uboreshaji wa miundombinu ya kilimo; utoaji wa elimu na ujuzi katika kilimo Pamoja na utoaji ruzuku kwenye bidhaa, zana, mbolea na pembejeo. Kama Afrika haitofikia makubaliano ya matumizi ya mbegu hizi, Mkataba wa AfCFTA utapungua manufaa. Afrika inapaswa kuamua.