Report ya Ukaguzi wa Uhuru wa Kiuchumi Tanzania 2025
Uhuru wa kiuchumi wa Tanzania upo katika hatua nyeti. Wakati nchi nyingine zinafungua mianya kwa masoko huru na ubunifu wa sekta binafsi, Tanzania imeelekea zaidi kwenye mfumo unaodhibitiwa na serikali. Hali hii inaonekana wazi katika Ripoti ya Uhuru wa Kiuchumi Duniani ya mwaka 2023, ambapo nchi ilipata alama 6.34 kati ya 10 na kushika nafasi ya 8 kati ya nchi 24 za Afrika Mashariki na Kusini, ikiwa chini ya viongozi wa mageuzi wa kikanda kama Rwanda na Mauritius. Licha ya uthabiti wa kiuchumi wa jumla na ukuaji wa wastani wa asilimia 5–6 tangu mwaka 2015, dalili za kusimama kimfumo zinaonekana wazi: nafasi kubwa ya serikali katika sekta za miundombinu, nishati na kilimo imepunguza kasi ya ubunifu na ushindani wa sekta binafsi. Kwa mfano, Tanzania bado ipo nyuma katika uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) ikilinganishwa na majirani zake, ambapo taarifa za UNCTAD (2023) zinaonyesha Rwanda ikivutia dola milioni 399 za Kimarekani, Uganda dola bilioni 1.5, huku Tanzania ikipata dola bilioni 1.1 licha ya kuwa na uchumi mkubwa zaidi.
Wakati huo huo, viwango vya Benki ya Dunia katika ripoti za Doing Business (kabla ya kusitishwa mwaka 2020) vilikuwa vikiiweka Tanzania chini ya majirani zake katika ufanisi wa udhibiti, hasa katika kuanzisha biashara na kupata vibali vya ujenzi. Hali hii inaonyesha kitendawili kikubwa: mageuzi mara nyingi hutangazwa na hata kuingizwa kwenye sheria, lakini utekelezaji wake kwa vitendo umekuwa dhaifu. Kwa hiyo, viashiria vya ukuaji wa uchumi vimekuwa vikisonga kinyume na mwelekeo wa uhuru wa kiuchumi. Kwa uhalisia, Tanzania inaonekana kuwa karibu zaidi na “Uhuru wa Kiserikali” kuliko Uhuru wa Kiuchumi. Serikali ndiyo inaongoza miradi ya maendeleo huku sekta binafsi ikilazimika kujipanga ndani ya mipaka iliyowekwa. Matokeo yake, ajenda ya maendeleo ya taifa imejikita zaidi katika nafasi ya serikali kuliko katika kufungua uwezo wa wananchi wake.
Licha ya utofauti uliopo kati ya mfumo wa kisheria na sera wa Tanzania (nadharia) na utekelezaji wake halisi (vitendo), viashiria vya ustawi wa kijamii wa hivi karibuni vinaonyesha jinsi kupungua kwa uhuru wa kiuchumi kunavyohusiana moja kwa moja na kudorora kwa matokeo ya maendeleo ya binadamu. Kwa mfano, mwaka 2022, kiwango cha usomaji kwa vijana nchini Tanzania kilikuwa takribani asilimia 87.1, chini kidogo ya Kenya yenye asilimia 87.8 na juu kidogo ya Rwanda yenye asilimia 86.5[1]. Kuhusu upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, mojawapo ya viashiria muhimu vya nishati safi, chini ya asilimia 10 ya Watanzania wanapata mafuta ya kisasa ya kupikia, ilhali nchini Kenya kiwango hicho kinakaribia asilimia 60 katika maeneo ya mijini[2]. Ajira za watoto bado zipo katika kiwango cha kutisha nchini Tanzania, ambapo 28.8% ya watoto wenye umri wa miaka 5–17 wanahusishwa katika ajira za watoto, ikilinganishwa na 8.5% pekee nchini Kenya[3].
Umaskini wa vipengele vingi (Multidimensional poverty) pia umeenea kwa kiwango kikubwa: zaidi ya 55% ya Watanzania wanakabiliwa na changamoto zinazoingiliana katika afya, elimu na viwango vya maisha, kiwango ambacho kiko juu zaidi kuliko kiwango cha 48.8% cha Rwanda katika kipimo kinachjulikana kwa kiingereza kama “Multidimensional Poverty Index” (MPI)[4]. Takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa viwango vya chini vya uhuru wa kiuchumi au utegemezi mkubwa wa mfumo unaoongozwa na serikali vina uhusiano wa moja kwa moja na kuzorota kwa maendeleo katika maeneo muhimu ya ustawi kama vile elimu ya kusoma na kuandika, upatikanaji wa nishati safi, kupunguza ajira za watoto na kupunguza umaskini. Katika ngazi ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, vikwazo ni wazi vilevile. Uchambuzi wa taarifa za FINSCOPE 2023 uliofanywa na waandishi wa taarifa hii unaonyesha kuwa takribani 85% ya watu waliohojiwa (kati ya takriban watu 9600), nchini Tanzania hawana hati miliki rasmi, jambo linalowazuia kutumia mali zao kama dhamana ya mikopo, pengo la sera ambalo Rwanda imefanikiwa kulitatua kupitia usajili wa ardhi wa karibu nchi nzima.
Wakati huohuo, uhalalishaji wa biashara nchini Tanzania uko katika kiwango cha chini sana kwani taafrifa hizo za FINSCOPE, 2023, zinaonyesha ni 7% pekee ya kampuni zinazofanya biashara ndizo zilizosajiliwa rasmi, ikilinganishwa na zaidi ya 20% nchini Kenya. Hali hii inadhoofisha ujasiriamali, upatikanaji wa fedha na ushindani wa kibiashara. Kwa ujumla, mapungufu haya katika ustawi wa kiuchumi wa kitaifa na vikwazo vya taasisi katika ngazi ya chini yanasisitiza jinsi kupungua kwa uhuru wa kiuchumi kunavyosababisha kusimama kwa maendeleo huku majirani wa kikanda wenye kasi kubwa ya mageuzi wakiwa tayari wanavuna matunda ya kijamii na ya kimaendeleo.
Makadirio yaliyowasilishwa katika muhtasari huu yametokana na mchanganyiko wa mbinu za kulinganisha, uchambuzi wa mwenendo na takwimu za maelezo, yakitumia hifadhitaarifa ya Taasisi ya Fraser (Fraser Institute’s Economic Freedom of the World -EFW), Kanzitaarifa ya Viashiria vya Maendeleo Ulimwenguni (World Development Indicators), Uchambuzi wa taarifa za FINSCOPE Tanzania 2023, pamoja na mashauriano ya kitaalamu na maafisa wa serikali wa ngazi za mbalimbali. Watafiti walilinganisha nafasi ya sasa ya Tanzania na nchi zinazotekeleza mageuzi kama Rwanda, Mauritius, na Vietnam, ambazo sera zao za kuachilia uhuru wa kiuchumi zimeleta mafanikio yanayopimika katika ukuaji na uwekezaji.
Halikadhalika, watafiti wakijikita kwenye tafiti za kimfumo zilizopo, ambazo zinaonyesha kuwa ongezeko la alama katika kipimo cha Uhuru wa Kiuchumi (EFW) lina uhusiano wa moja kwa moja na kasi kubwa ya ukuaji wa pato la taifa (GDP), kupungua kwa umaskini, na ongezeko la uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, uchambuzi huu umetumia uhusiano huo katika muktadha wa Tanzania. Mbinu ya kulinganisha ilitumika kukadiria athari za mageuzi makubwa katika maeneo matano ya kipaumbele. Kwa msingi huo, uchambuzi wa mwenendo unaonyesha kwamba kwa kusukuma mbele mageuzi, Tanzania inaweza kufikia upungufu wa umaskini kwa kasi ya hadi 15% zaidi, kuongeza kasi ya ukuaji wa pato la taifa (GDP) kwa takribani pointi 1.2 za asilimia kwa mwaka ukilinganisha na sasa, na kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje wenye thamani ya dola bilioni 4.8 ifikapo mwaka 2030. Takwimu hizi hazipaswi kuchukuliwa kama utabiri kamili, bali kama hali halisi zinazowezekana, zilizoegemea kwenye ushahidi wa kimataifa na kurekebishwa kulingana na mazingira ya kiuchumi ya Tanzania.
Kitendawili cha Mkwamo wa Uhuru wa Kiuchumi wa Tanzania
Wakati Tanzania imeendelea kudumisha uthabiti wa kiuchumi wa jumla, bado inafanya vibaya katika nguzo kuu za uhuru wa kiuchumi. Kinyume chake, majirani kama Rwanda na Kenya wamefanya mageuzi makubwa na sasa wanavutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) mara tatu zaidi kwa kila mtu ikilinganishwa na Tanzania. Kati ya mwaka 2015 na 2022, alama ya Tanzania katika kipimo cha “Ukubwa wa Serikali” ilishuka kwa pointi 1.4 na sasa ipo katika 6.1. Viashiria vya “haki za umiliki na mfumo wa sheria” vimeendelea kukwama katika 5.05, na kuiweka nchi katika nafasi ya 6 kikanda, ikiwa na mabadiliko madogo zaidi miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Kipimo cha “Uimara wa Fedha” kilipanda kidogo hadi 7.43, lakini kuanzia mwaka 2021 kimeanza kushuka. Uhuru wa Biashara Kimataifa Uliopo (Freedom to Trade Internationally) uko katika kiwango cha chini cha 6.05, nafasi ya 15 kati ya nchi 24 katika maeneo ya EAC na SADC, na nguzo ya Udhibiti (Regulatory pillar) ipo chini ya wastani wa kikanda katika 6.24 licha ya maboresho madogo baada ya mwaka 2022.
Uthibitisho wa Miliki za Ardhi
Nyuma ya alama hizi kuna changamoto za kivitendo zilizoota mizizi kwa muda mrefu. Utafiti wa FINSCOPE Tanzania 2023 unaonyesha kuwa takribani 85% ya wamiliki wa ardhi walihojiwa wanamiliki ardhi kwa njia zisizo rasmi, hali inayowazuia kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana. Cha kushangaza ni kwamba ni 4% pekee ya watu wazima wana Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), na chini ya 7% ya biashara zimesajiliwa rasmi. Zaidi ya nusu ya waliohojiwa (51%) huzungumzia masuala ya kifedha ndani ya kaya pekee, jambo linaloashiria ushiriki mdogo katika masuala ya kifedha. Ukosefu wa ufanisi katika mifumo ya udhibiti pia una athari kubwa, kwani biashara ndogo na za kati (SMEs) hupoteza hadi siku 22 kwa mwaka kufuatilia masharti ya uzingatiaji (regulatory controls). Haya siyo matatizo madogo ya kiutawala; ni vizuizi vya kimuundo vinavyoweza kushughulikiwa kupitia mageuzi mahsusi ya sera.
Vikwazo Vinavyoendelea na Hatari Zinazojitokeza
Licha ya ukuaji thabiti wa Pato la Taifa (GDP) na uwekezaji katika miundombinu, Tanzania bado imeainishwa kama “nchi isiyo huru kwa kiasi kikubwa,” ikiwa na wastani wa alama 6.34/10 katika kipimo cha EFW, na kushika nafasi ya 8 kati ya nchi 24 za Afrika Mashariki na Kusini. Utendaji huu wa kati unaficha changamoto za msingi zinazozuia ubunifu na ujasiriamali kama ilivyofupishwa hapa chini;
- Kwanza, kuongezeka kwa nafasi ya serikali katika uchumi kupitia mashirika ya umma (State Owned Enterprises -SOEs), ruzuku, na viwango vya juu vya kodi kumeendelea kuziba nafasi ya uwekezaji na ubunifu wa sekta binafsi. Tangu mwaka 2015, kwa wastani alama ya Tanzania katika kipimo cha “Size of Government” imeshuka kwa pointi 0.75, huku ruzuku pana na mzigo unaoongezeka wa kifedha vikifuta mafanikio ya awali ya mageuzi ya kiuchumi.
- Pili, haki za umiliki na mfumo wa kisheria bado ni dhaifu. Ingawa Tanzania ina moja ya viwango vya chini zaidi vya mabadiliko (stability) katika alama za mfumo wa kisheria katika ukanda huu, “utulivu” huo unaficha mkwamo. Ukosefu wa uhuru wa mahakama, ucheleweshaji wa utekelezaji wa mikataba, na ukosefu wa sheria zenye kuzingatia usawa wa kijinsia ni vikwazo vikubwa kwa umiliki salama wa ardhi na ujasiri wa wawekezaji. Kama ilivyoelezwa hapo juu, zaidi ya 85% ya wamiliki wa ardhi waliomo katika utafiti wa FINSCOPE walipata ardhi yao kwa njia zisizo rasmi na hawana hati yoyote rasmi inayothibitisha umiliki wao, jambo linalowaathiri zaidi wanawake na jamii za vijijini.
- Tatu, kuyumba kwa uthabiti wa fedha katika kipindi cha hivi karibuni na kuendelea kuwepo kwa udhibiti wa akaunti za fedha za kigeni kunadhoofisha uhakika wa uwekezaji na uimara wa kaya. Wakati Tanzania inaendelea kudhibiti mabadiliko ya bei (inflation volatility) kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na majirani zake, mageuzi ya kimuundo yanahitajika ili kuimarisha uhuru wa benki kuu na kupanua upatikanaji wa huduma za akiba na uwekezaji.
- Nne, uhuru wa biashara wa Tanzania umepungua kwa kasi, hasa tangu mwaka 2010. Nguzo hii ambayo inafanya vibaya zaidi imezoroteshwa na ukosefu wa ufanisi katika forodha, udhibiti wa mtaji, na vizuizi visivyo vya ushuru (NTBs) vinavyowatenga wazalishaji wa ndani na masoko ya kimataifa. Nchi jirani kama Rwanda na Kenya zinaendelea kwa kasi zaidi katika kuwezesha biashara.
- Tano, ukosefu wa ufanisi katika mifumo ya udhibiti unaendelea kuathiri biashara ndogo na za kati (SMEs), wajasiriamali wanawake, na biashara zisizo rasmi. Takwimu za FINSCOPE zinaonyesha kuwa ni 7% pekee ya biashara zilizosajiliwa rasmi, na gharama za uzingatiaji bado ni kubwa kupita kiasi kutokana na mifumo isiyounganishwa na kanuni ngumu za ajira. Vikwazo katika ngazi ya chini kama urasimu wa upatikanaji wa hati miliki, mifumo ya kidijitali isiyoratibiwa (mfano BRELA na TRA), na taratibu za mikopo zisizojumuisha vikundi vyote vinazidisha ukosefu wa usawa na kukwamisha ukuaji wa biashara.
Ajenda ya Mageuzi Kulingana na Nguzo Mahususi
Ili kuondoa mkwamo na kufungua ukuaji jumuishi, mageuzi yanapaswa kuanza kwa kupunguza ukubwa wa ushawishi wa serikali katika uchumi. Matumizi ya umma, hasa kupitia mashirika ya umma (SOEs) na ruzuku, yamepunguza alama ya kipimo cha ukubwa wa serikali. Hatua muhimu ni pamoja na kubinafsisha mashirika yasiyo ya kimkakati kama TTCL kufikia mwaka 2026, kubadilisha ruzuku za jumla kuwa misaada ya kifedha ya moja kwa moja kupitia simu za mkononi, na kupunguza kiwango cha juu cha kodi ya mapato (income tax) kutoka kati ya 30–45% hadi takribani 20%. Mageuzi haya yanakadiriwa kuongeza alama ya EFW kwa pointi 1.5, hivyo kuachia fedha za umma zitakazotumika katika kuboresha mfumo wa mahakama na mifumo ya umiliki wa mali kidigitali. Hata hivyo, kupunguza ushawishi wa serikali ni suala linalohusiana na mageuzi ya kikatiba kwa sababu kupunguza ukubwa wa serikali mara moja pekee hakumaanishi moja kwa moja kuongezeka kwa uhuru wa kiuchumi; yote yanategemea athari endelevu zinazofuata. Ni lazima kuwe na sekta binafsi yenye uwezo wa kuchukua jukumu la serikali katika maeneo ambayo Serikali haipaswi kushiriki ama hakuna ulazima. Kwa mfano, endapo mashirika ya umma yanajihusisha na uzalishaji wa bidhaa za watumiaji ambazo sekta binafsi inaweza kuzalisha, basi uwezo na utayari wa sekta binafsi vinapaswa kutathminiwa ili kuepuka kurudia changamoto zilizojitokeza wakati wa ubinafsishaji wa mwishoni mwa miaka ya 1990. Vinginevyo, njia ya ubinafsishaji wa hatua kwa hatua kama ilivyotekelezwa Mauritius inaweza kuzingatiwa kwa mashirika yasiyo na ufanisi.
Pili, kuimarisha haki za umiliki ni jambo la msingi. Mchakato wa kidijitali wa hatua tatu (kupima, kusajili na kumilikisha) wa usajili wa hati za ardhi unaweza kuwafikia kaya 85% ambazo kwa sasa hazina umiliki rasmi. Mchakato huu wa hatua tatu kwa kawaida unahusisha kidigitali nyaraka za ardhi zilizopo kwenye karatasi, kuunda jukwaa la mtandaoni kwa ajili ya usimamizi wa ardhi, na kuweka mfumo salama na wazi wa miamala ya ardhi. Mageuzi ya kisheria yatakayolinda haki za urithi za wanawake na kuanzishwa kwa mahakama maalum za kiuchumi katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi (Special Economic Zones -SEZs) yataimarisha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa haki na usalama wa mali za wawekezaji. Mabadiliko haya yanaweza kusababisha kupungua kwa umaskini kwa hadi 15% na kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi tatu bora katika ukanda huu kwa viashiria vya haki za umiliki.
Mageuzi katika biashara na uwekezaji pia ni ya dharura. Wauzaji wa bidhaa nje ya nchi kwa sasa wanapoteza takribani 14% ya mapato yao kutokana na ukosefu wa ufanisi mipakani na vizuizi visivyo vya ushuru (NTBs). Tanzania inapaswa kupitisha jukwaa la kidijitali la forodha lililounganishwa kikanda ifikapo katikati ya mwaka 2026, kuondoa vizuizi visivyo vya ushuru vilivyobainishwa, na kuzindua mpango wa “Export Tanzania” utakaotumia akili mnemba (AI) kubaini masoko bora na kuboresha ufuatiliaji wa bidhaa za kilimo. Hatua hizi zinaweza kuongeza mauzo ya nje ya bidhaa zilizochakatwa na nguo kwa takribani 25%.
Ukuaji wa biashara unakwamishwa na mifumo iliyogawanyika na ukosefu wa uwazi. Jukwaa la Kitaifa la Huduma za Biashara “One-Stop Business Portal” litakalounganisha BRELA, TRA, na mamlaka za serikali za mitaa lingeweza kurahisisha taratibu za usajili na utoaji vibali. Leseni zitakazotolewa kwa mfumo wa tathmini ya hatari zenye upyaishaji wa kiotomatiki, pamoja na utekelezaji kamili wa Rejesta ya Dhamana ya Mali Zinazohamishika (Movable Collateral Registry), vitapunguza gharama za uzingatiaji na kufungua upatikanaji wa mikopo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs)[5]. Kwa pamoja, hatua hizi zinaweza kuongeza kiwango cha usajili rasmi wa biashara mara tatu kufikia mwaka 2027.
Pengo la mikopo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) kwa sasa linakadiriwa kufikia dola bilioni 2.3, huku uelewa wa masuala ya kifedha ukiendelea kuwa mdogo. Suluhisho linajumuisha kuwezesha usajili wa TIN kupitia misimbo ya simu ya USSD, kuanzisha mfumo wa kitaifa wa kidijitali wa kupima uwezo wa mikopo unaotegemea taarifa za miamala ya fedha za simu, na kutoa hati fungani za akiba zinazolinganishwa na mfumuko wa bei ambazo zinapatikana kupitia pochi za simu. Hatua hizi zinaweza kuongeza utoaji wa mikopo rasmi kwa SMEs kwa takribani 40% na kuimarisha ustahimilivu wa kifedha wa kaya.
Vipaumbele vya Mageuzi na Hatua za Kimkakati
Ukaguzi huu unatambua maeneo matano muhimu ya mageuzi, kila moja likiambatana na hatua za kimkakati zinazolenga kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa Tanzania na uwezo wa utawala bora.
- Kwanza, chini ya kipengele cha Ukubwa wa Serikali, ripoti inapendekeza ubinafsishaji wa kimkakati wa mashirika ya umma (SOEs) yasiyo ya kimkakati katika sekta kama nishati na mawasiliano. Pia inapendekeza kubadilisha ruzuku za jumla kuwa misaada ya kifedha ya moja kwa moja kwa walengwa mahsusi ili kulinda makundi yaliyo hatarini huku ikihakikisha uimara wa kifedha wa taifa. Zaidi ya hayo, inapendekezwa kupunguza kiwango cha juu cha kodi ya mapato kutoka kiwango cha sasa cha 30–45% hadi 30% pekee ili kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi.
- Pili, katika eneo la Mfumo wa Kisheria na Haki za Umiliki, ajenda ya mageuzi inajikita katika kutekeleza mageuzi ya kikatiba na ya kimahakama ili kuhakikisha ulinzi thabiti zaidi wa haki za umiliki. Kipaumbele ni kidigitali usajili wa hati za ardhi kuanzia na miradi ya majaribio katika mikoa mitano, sambamba na kukuza usawa wa kijinsia kupitia mageuzi ya umiliki wa pamoja wa ardhi na mapitio ya sheria za familia/ndoaa kwa lengo la kulinda haki za wanawake katika umiliki wa ardhi.
- Tatu, kuhusu Sarafu Imara, ripoti inasisitiza umuhimu wa kuimarisha uhuru wa Benki Kuu ya Tanzania ili kuunga mkono utekelezaji wa sera za fedha zinazolenga kudhibiti mfumuko wa bei. Kuongeza upatikanaji wa hati fungani za akiba zinazolinganishwa na mfumuko wa bei kwa kaya na kulegeza kanuni za udhibiti wa akaunti za fedha za kigeni ni hatua muhimu pia. Aidha, inapendekezwa kuhimiza bidhaa za akiba zinazotegemea simu za mkononi ili kupanua ujumuishaji wa kifedha.
- Nne, chini ya kipengele cha Uhuru wa Biashara ya Kimataifa, ukaguzi unapendekeza kuunganishwa kikamilifu na jukwaa la kidijitali la forodha la pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kuboresha urahisishaji wa biashara. Pia unasisitiza kuondolewa hatua kwa hatua kwa vizuizi visivyo vya ushuru, kurahisishwa kwa taratibu za forodha, na utekelezaji wa mpango wa “Export Tanzania.” Mpango huu utalenga kusaidia sekta za kuongeza thamani na kutumia mifumo ya ufuatiliaji inayowezeshwa na akili mnemba (AI) kusaidia wauzaji nje wa Tanzania kuzingatia viwango vya masoko ya Umoja wa Ulaya.
- Mwisho, katika kipengele cha Ufanisi wa Udhibiti, mpango wa mageuzi unapendekeza kuanzishwa kwa jukwaa moja la kidijitali lililounganishwa litakalojumuisha huduma kutoka BRELA, TRA, na taasisi nyingine za serikali kuu na za mitaa ili kurahisisha usajili wa biashara na uzingatiaji wa kanuni. Hatua nyingine muhimu ni pamoja na kutekeleza mifumo ya utoaji leseni kulingana na tathmini ya hatari, kuruhusu upyaishaji wa kiotomatiki kwa biashara zenye hatari ndogo, na kufanya mapitio ya kanuni za ajira ili kutoa unafuu kwa biashara ndogo huku vibali vya kazi kwa wawekezaji wa kigeni vikitolewa kwa haraka zaidi.
Matokeo Yanayotarajiwa
Iwapo mageuzi yaliyopendekezwa yatatekelezwa kikamilifu, yanaweza kubadilisha kabisa mazingira ya kiuchumi ya Tanzania. Ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) wa kila mwaka utaongezeka kwa pointi 1.2 za asilimia. Umaskini utapungua kwa kasi ya 15% zaidi, hasa katika maeneo ya vijijini. Zaidi ya ajira rasmi 600,000 zitaanzishwa, na upatikanaji wa nishati safi utaongezeka kwa 30%, hatua ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto za kimazingira na kijamii. Uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje unaweza kuongezeka kwa dola bilioni 4.8, na ajira za watoto wa kike zinaweza kupungua kwa 40%, huku usawa kamili wa kijinsia katika kiwango cha kusoma na kuandika ukiwa unaweza kufikiwa ifikapo mwaka 2030. Makadirio haya yanatokana na tafiti za nchi mbalimbali zinazochambua mwenendo wa kiuchumi kwa kutumia taarifa za WDI na EFW[6]. Iwapo mageuzi haya yatatekelezwa, yanaweza kuleta matokeo yanayopimika:
- Kupanuka kwa Sekta Binafsi: Kupunguzwa kwa mizigo ya udhibiti na kodi kutachochea ujasiriamali rasmi, uundaji wa ajira, na uwekezaji wa ndani.
- Ujumuishaji wa Kifedha: Mageuzi katika mifumo ya dhamana na kulegezwa kwa udhibiti wa fedha za kigeni yataongeza upatikanaji wa mikopo na fursa za akiba, hasa kwa wanawake na kaya za vijijini.
- Ushindani wa Kikanda: Kuboresha urahisishaji wa biashara na maandalizi ya mauzo ya nje kutasaidia Tanzania kuendana na maendeleo ya Rwanda, Mauritius na Kenya.
- Kupunguza Umaskini na Usawa wa Kijinsia: Mageuzi ya haki za umiliki, kulegeza kanuni, na upatikanaji wa nishati safi yataharakisha maendeleo katika kupunguza umaskini na kuimarisha usawa wa kijinsia.
Hitimisho
Uhuru wa kiuchumi wa Tanzania umeendelea kuwa thabiti, lakini uthabiti huo umekuja kwa gharama ya mkwamo. Wakati nchi nyingine za ukanda huu zimeharakisha mageuzi ya kiuchumi huria, Tanzania imekuwa ikirudi nyuma tangu mwaka 2015 katika uwazi wa biashara na ukubwa wa serikali, jambo linalohatarisha kuzidisha utendaji duni wa kiuchumi. Kinachohitajika sasa ni mwelekeo thabiti wa kuhamia kutoka katika maendeleo yanayoongozwa na serikali yenye miradi mizito ya miundombinu kwenda kwenye mageuzi yanayozingatia nguvu ya soko na taasisi imara. Mapendekezo yaliyotolewa katika ukaguzi huu hayatoi ukosoaji pekee, bali ramani ya njia ya kuibadilisha Tanzania kutoka “nchi isiyo huru kwa kiasi kikubwa” hadi kuwa kinara wa kikanda katika uhuru wa kiuchumi. Ili mabadiliko yawe na maana, mageuzi yanapaswa kuwa jasiri, jumuishi, na yenye kuzingatia kwa uthabiti kufunguliwa kwa fursa katika kila ngazi ya jamii.
Mustakabali wa Tanzania hautaamuliwa na miundombinu pekee bali na ubora wa taasisi zake. Msisitizo mkubwa katika ujenzi wa miundombinu lazima uende sambamba na msisitizo sawia katika kuimarisha taasisi za kijamii na kiuchumi zinazochochea matumizi bora na yenye tija ya miundombinu hiyo. Kufikia ustawi jumuishi kunahitaji kuondoa vikwazo vya kimuundo vilivyojikita kwa muda mrefu vinavyowatenga wanawake, vijana, kaya za vijijini, na biashara ndogo dhidi ya ushiriki wenye maana katika uchumi. Iwapo mapendekezo yaliyo hapo juu yatatekelezwa kwa dharura na kwa nia ya kisiasa ya dhati, mageuzi haya yanaweza kuifanya Tanzania isiwe tu na uchumi imara, bali pia kuwa kinara wa kikanda katika uhuru wa kiuchumi ifikapo mwaka 2030.
[1] TheGlobalEconomy.comMaxinomics+1
[4] cdn.sida.seUN Trade and Development (UNCTAD)
[5] Kwa sasa, muswada wa sharia kuhusu jambo hilo umekamilika. Unaweza kuangalia hapa, https://polis.bunge.go.tz/uploads/bills/1770366301-Muswada_wa_Sheria_ya_Mikopo_kwa_Dhamana_za_Mali_Zinazohamishika_wa_Mwaka_2026.pdf
[6] Katika kuunga mkono matokeo yaliyowasilishwa katika ripoti hii, miswada mitano ya kuchapishwa iko chini ya hatua tofauti za maendeleo na masasisho yanaweza kupatikana kutoka kwa waandishi. Haya ni kama ifuatavyo;
- Nurdin Igangula & Samwel S. Alananga, “Uhuru wa Kiuchumi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara: Kupunguza Athari za Serikali Kutumia Uhuru kwenye Ukuaji”
- Samwel S. Alananga, “Ubora wa Kitaasisi na Ukuaji wa Uchumi katika Nchi Maskini “2024”: Je, Kanuni za Soko Zilizoboreshwa zina Athari yoyote?
- Rosemary Mnongya na Samwel S. Alananga, “Athari za Uhuru wa Kiuchumi kwa Ustawi: Je, Sauti ya Pesa Ni Muhimu Kweli?”
- Rashid A. Rashid & Samwel S. Alananga, “Ukuaji wa Ubora wa Kitaasisi na Uchumi katika Nchi Maskini “2024”: Je, Kanuni za Soko Zilizoboreshwa zina Athari yoyote?
- Mboni M. Kibelloh & Samwel S. Alananga, “Ubora wa Kitaasisi na Maendeleo ya Kiuchumi katika Nchi Maskini: Je, Kuimarishwa kwa Uhuru wa Biashara Kimataifa kuna Athari yoyote?”
Download the full report here
Liberty Sparks – Report Presentation
1.1_Economic Freedom Audit Report_final_1.1_Eng
1.2_Economic Freedom Audit Report_final_1.1_Sw
2.1_ECONOMIC FREEDOM POLICY PAPER 2025_Eng
2.2_ECONOMIC FREEDOM POLICY PAPER 2025_Sw
3.1_ECONOMIC FREEDOM AUDIT FOR TANZANIA 2024_MATRIX_Eng
3.2_ECONOMIC FREEDOM AUDIT FOR TANZANIA 2024_MATRIX_Sw
